Mji wa kale uliozama kuwa kivutio Mafia
Kisiwa cha
Mafia kipo katika mlango wa Mto Rufiji kusini mwa Tanzania. Maeneo ya kuvutia
ya mazingira ya bahari yametokea kujulikana zaidi haswa mara baada ya
kuanzishwa Hifadhi ya Bahari (Mafia Island Marine Park - MIMP) na Maeneo
Tengefu.
Kisiwa hiki
kipo umbali wa kilomita 135 kutoka Dar es Salaam na huchukua dakika 35 kwa
kutumia ndege ndogo kufika hapo.
Unapotafuta
habari za Kisiwa cha Mafia kwenye mitandao hukupeleka kwenye taarifa za vivutio
vya utalii pekee ambavyo vinajenga sura ya kisiwa hiki kuwa ni pepo ya watalii.
Kisiwa hiki ni sehemu ya wilaya sita za mkoa wa
Pwani. Kinachokadiriwa kuwa na wakazi 40,800 wanaotegemea kilimo na uvuvi.
Kutokana na historia
kinavutia watalii wanaofika kisiwani humo kwaajili ya fungate, kutazama pomboo
na uvuvi wa kujirufahisha.
Hivi karibuni karibuni katika
kisiwa hiki ambacho historia yake iliyo katika maandishi inaanzia karne ya
nane, kilipamba vichwa vya habari baada ya kugundulika uwepo wa mji uliozama
baharini.
Habari hii iliibua mjadala
huku upande mmoja ukisema inawezekana kweli mji huo ulizama na mwingine ukisema
ni maajabu tu ya Mungu na kwamba maji yametengeneza mfano wa mji.
Mjadala huu unazidi
kukitangaza Kisiwa hiki na utazidi kuvutia watalii kutoka kila kona ya dunia
kujionea ajabu hili.
Ugunduzi huo unaonekana
utakuza zaidi utalii kwa kuwa watafiti wanamiminika na watalii vilevile kila
mmoja akitaka kupata ukweli.
Wengine wanasema
inawezekana mji huo ulizama miaka 500 kutokana na mwonekano wa matumbawe yaliyojipachika
katika kuta zilizoanguka.
Lakini mtandao wa Ancient-origins unasema inawezekana mji
huo ni Raphta uliokuwa ukikaliwa na Warumi katika karne ya kwanza.
Mtandao huo unamnukuu
Mtaalamu wa Mambo ya Kale ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Felix Chami kuwa muonekano wa mabaki hayo unafanana na maelezo yaliyopo katika
nyaraka za Warumi.
Mji wa Raphta ambao ulikuwa
maarufu kwa biashara katika karne ya kwanza, ulionekana katika nyaraka na kwa
miaka mingi wataalamu wa kale wamekuwa wakitafuta ukweli.
Kwa mujibu wa Allan Sutton
baada ya kuruka na helikopta aliona uwapo kitu kisicho cha kawaida na kwamba
maji yalikuwa yakigawanyika kwa namna iliyompa shauku ya kutaka kujua zaidi.
Sutton na wenzake baadaye
walifanikiwa kulitembelea eneo hilo wakati wa maji kupwa wakiwa na mashua na vifaa
vya kupiga mbizi na kufanikiwa kulichunguza na kulipiga picha.
Katika utafiti wao huo
waliona kitu kinachoonekana kama misingi inayozunguka eneo kubwa. Katika
misingi hiyo kulionekana kuta kubwa za sarufi za mita tano na zaidi.
Msingi wa majengo hayo
upande wa kaskazini na kusini una wastani wa kati ya urefu wa kilometa 3.7 ila wanaamini kwamba kuna misingi mingine
ambayo hawakuiona ambayo imefunikwa na mchanga. Na hatua zaidi za kitaalamu
zinatakiwa kuchukuliwa ili kubaini hali ya hapo.
Anasema katika blogu yake
kwamba katika maeneo mengine upo upana mkubwa wa kiasi cha kilometa moja huku
kina chake kikiwa ni kati ya mita 12 hadi 20.
Sutton anasema kuta zinafanana na mchanga
lakini ukitazama karibu ni kama vile zimejengwa na saruji na katika kumeonekana
matundu ambayo huenda ni madirisha au milango.
No comments:
Post a Comment