Uvivu wa
kufikiri umeua biashara ya filamu Tanzania
Kama Wabongo
tungekuwa tunajua kupuuzia mambo ya ovyo kama tunavyofanya katika mambo ya
msingi basi nchi hii ingekuwa mbali.
Nguvukazi
nyingi inapotea katika mambo yasiyo na maana. Sina haja ya kuyataja mambo
yanayotuchukulia muda wetu mwingi na pesa.
Wapenzi na
wadau wa filamu walipokuwa wakipiga kelele kuhusu mustakabali wa tasnia hiyo,
wahusika waliwapuuza kila mmoja akajifanya yuko bize akirekodi filamu.
Wasanii wengi
walijidanganya kuwa mbona filamu zinatoka na umaarufu wao unakua kila siku,
lakini wenye akili walikaa pembeni wakipiga kelele kuwa njia waliyokuwa
wakipita haikuwa sahihi.
Wengine
waliwaandalia mafunzo mbalimbali, lakini wao walijidanganya kuwa anayeandaa
mafunzo hayo si maarufu kama wao, iweje ajifanye anajua zaidi ya wao.
Hata
yalipoandaliwa matamasha ya filamu waliyapuuza, walijiona kuwa juu ya kila kitu
ndio maana hawakuona umuhimu wa kuvifuatilia.
Sasa gwaride
limepigwa nyuma geuka, kila msanii anatafuta pakushikilia hapaoni. Ni sawa na
kusema kile walichokuwa wanajivunia sasa hakipo tena.
Wasanii
wengi sasa hivi hawapo tena lokesheni kama wanavyopaita. Wengi wanaganga njaa
katika mambo mengine, waliobahatika sasa wanafanya biashara zao wale wengine
wanabaki kuruka huku na kule kuvizia filamu chache zinazoendelea kuzalishwa.
Sasa hivi
wakiitwa kucheza filamu za wasanii chipukizi kwa ujira wa Sh150,000 wanakwenda.
Watafanya nini? Hawana ujanja tena.
Yote kwa
yote mchawi wa soko la filamu nchini ni wasanii wenyewe kwa kuwa waliposhika hatamu
hawakukumbuka kuwa wanaweza kushuka.
Katika kazi
au biashara, hakuna kinachoweza kubaki juu milele kama haitakuwepo mipango
thabiti. Yaani isingewezekana soko la filamu likabaki vilevile wakati watu ni
walewale na kinachofanyika ni kilekile miaka yote.
Hakuna
miujiza katika mafanikio. Tumeikuta Hollywood na tutakufa tukiicha na ubora
wake. Ile haikushushwa kama neno la Mungu. Pale kuna watu wanakesha wakiumiza
kichwa na kufanya kazi nini wafanye ili waendelee kushika hatamu.
Wengine
wanafanya utafiti kujua nini wafanye ili waendelee kututawala kifikra kupitia
filamu. Zipo filamu zilitengenezwa miaka 40 iliyopita lakini ukitazama ubora
wake na utunzi ni zaidi ya ile itakayotolewa kesho na mtayarishaji wa
Bongomovie.
Tatizo ni
kutotaka kuwekeza nguvu katika mambo ya msingi. Wasanii walipoanza kupata pesa
kupitia filamu ulikuwa mwanzo wa matatizo yao.
No comments:
Post a Comment